Wiki hii Serikali ilikuwa kwenye mapambano mengine na wanafunzi wa vyuo vikuu ambao waliamua kugoma wakishinikiza kulipwa fedha zao za kujikimu ambazo kiutaratibu zinatoka Bodi ya Mikopo ambayo imedaiwa kuchelewesha fedha hizo kwa zaidi ya wiki 11.
Mbali na kugoma, wanafunzi hao walifanya fujo kwenye Kampasi ya Mabibo na kuharibu vitu kadhaa ambavyo wanatakiwa kuendelea kuvitumia baada ya mgomo kumalizika.
Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Mwigulu Mchemba alitoa tamko kwa niaba ya Serikali akiomba radhi kwa kuchelewesha fedha hizo na kuwahakikishia wanafunzi kuwa fedha hizo zitaingia mara moja kwenye akaunti zao na kuwasihi kuendelea na masomo.
Hata hivyo, wanafunzi hao waliendelea na mgomo hadi utashi wao ulipotimizwa. Mgomo huo haukuhusu wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pekee, bali ulisambaa sehemu nyingine zote, wakiwamo wanafunzi 15 wa Chuo Kikuu cha Dodoma waliokamatwa baada ya kufanya fujo wakati wakidai haki zao.
Pia wanafunzi 400 wa Chuo Kikuu cha Mt Joseph cha jijini Dar es Salaam pia walisimamishwa masomo baada ya kuingia kwenye mgomo wakidai fedha zao za kujikimu zilizocheleweshwa.
Mara kadhaa matatizo haya ya wanafunzi kucheleweshewa fedha zao yamekuwa yakiibuka na imekuwa ni kawaida kwa Serikali kutumia vyombo vyake vya dola kuwatuliza, huku baadhi wakikamatwa na kufunguliwa kesi au kuachiwa kwa tuhuma za kukiuka sheria wakati wa kudai haki zao.
Hata hivyo, matatizo yanapoisha na jitihada za kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo yao huishia hapo hapo hadi tatizo jingine linapozuka. Kibaya zaidi ni pale Jeshi la Polisi linalolazimishwa kutumia nguvu za ziada katika kudhibiti wanafunzi na kusababisha baadhi kujeruhiwa, kupotezewa muda zaidi wa masomo na hata kujenga chuki dhidi ya Serikali yao.
Tunadhani kuwa hiyo siyo sahihi kwa sababu haki ya kugoma na kuandamana ni haki ya kimsingi ya kila raia pale anapotaka jamii ijue kile kinachomkera au kumfurahisha. Kwa maana hiyo, maandamano yote ya kupinga au kupongeza, mgomo ni haki ya kila raia, lakini inatakiwa iwekewe utaratibu tu wa kuitekeleza.
Kuzuia maandamano hakutatui matatizo ya wanafunzi na kutumia nguvu za ziada kudhibiti wanafunzi wanaogoma hakutatui matatizo yao. Kinachotakiwa ni Serikali kujipanga kuhakikisha matatizo hayo hayaibuki na kusababisha wanafunzi watumie haki yao ya kugoma au kuandamana.
Wanafunzi kukaa wiki 11 bila ya kupata fedha za kujikimu siyo kitu kidogo na kwanza walistahili kupongezwa kwamba waliweza kuvumilia kwa kipindi kirefu kuishi bila ya fedha za kununulia hata sabuni. Hapa waliosababisha tatizo hilo ndiyo walistahili kuchukuliwa hatua kwanza badala ya wanafunzi.
Hawa watu waliotakiwa kupeleka fedha za wanafunzi lakini wakachelewa kwa wiki 11, wanaendelea kufanya kazi zao wakilipwa mishahara kutokana na kodi za wananchi bila ya kuguswa na kirungu wala kufunguliwa mashtaka, badala yake waziri anajitokeza kuwaombea radhi. Utamaduni huu hauwezi kutuletea mabadiliko.
Inashangaza kuona kwamba hadi leo aliyechelewesha fedha hizo ameachwa bila ya hata kutingishwa wakati waliogoma hadi kufanya fujo kutokana na kucheleweshwa kwa fedha hizo wamesimamishwa masomo, kupigwa na hata kufunguliwa mashtaka. Kwa utamaduni huu nchi itakwenda kweli?
Pamoja na hayo, wanafunzi pia wanatakiwa waanike matatizo yao kwa njia ambayo haitaharibu miundombinu ambayo wanaitumia kwenye masomo na ambayo itatumiwa na vizazi kadhaa vijavyo. Kufanya fujo na uharibifu ni kutowajibika pia kwa nchi yao na vizazi vinavyowafuata.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni