Social Icons

Jumapili, 24 Novemba 2013

MBINU ZA KUACHA UVUTAJI SIGARA

Miongoni mwa mambo magumu kabisa katika ufanikishaji wake ni mtu kuachana na uvutaji wa sigara. Watu wengi wamekuwa wakionywa kuachana na uvutaji wa sigara kwa sababu ya madhara yake, lakini wamekuwa wakishindwa kutokana na kukolewa na kiwango cha Nikotini inayopatikana katika tumbaku.

Vijana wengi wamekuwa wakijiingiza katika uvutaji kwa kufuata mkumbo, lakini baadaye wanapokuja kutambua kuwa wako katika hatari ya kuambukizwa au pengine wana ugonjwa wa kifua kikuu, wanakuwa katika wakati mgumu wa kuachana na uvutaji huo. Wengi wao wamekufa huku makundi kwa makundi wakitangatanga kutafuta suluhu ya kuchana na uvutaji, si tu kwa sababu ya kuhofia ugonjwa, bali hata kukosa uwezo wa kununua bidhaa hiyo.

Hata hivyo idadi kubwa ya wanaojaribu kuacha wamejikuta wakipata majibu ya kutoweza, kutokana na kusumbuliwa na hamu ya uvutaji, umbumbu wa mawazo pindi wanapokaa muda mrefu bila kuvuta, kuumwa na kichwa na hata udhaifu katika kukumbuka vitu au mambo waliyofanya au waliyopanga kuyatenda.

Pamoja na yote hayo watalaam na washauri wa masuala uvuaji wa sigara wanasema wanaopatwa na hayo wamekosa mbinu na muongozo wa kuwasaidia waachane na uvutaji wa sigara bila kupata madhara.

Kwa ufupi somo hili limehusisha uchunguzi wa kina pamoja na kumbukumbu za kitaalamu kutoka kwa washauri kama Anderson JE, Jorenby DE, Scott WJ, Fiore MC, Bailey WC, Cohen SJ, ambao wote kwa pamoja kupitia vituo vyao kikiwemo cha US Department of Health and Human Services na Public Health Service walishawahiwa kueleza mbinu salama za kuachana na uvuaji wa sigara. Zifuatazo ni dondoo kadhaa za kufuata ili mvutaji aache sigara kwa usalama.

* Mvutaji lazima afahamu ni muda gani ambao huwa anavuta sigara kwa wingi, je ni wakati akiwa amelewa au akiwa na mawazo mengi ya kimaisha? Akishafahamu hilo ajiulize ni kiwango gani cha sigara ambacho huwa unavuta kwa siku?

* Baada ya hapo achukua kitabu chake cha kumbukumbu na aandike muda huo ambao yeye huvuta sigara kwa wingi. Ajiulize kwa nini huwa unavuta, atathimini madhara ya uvutaji wa sigara kwake binafsi na kwa familia yako.

* Kaa chini upitie kwa makini kumbukumbu zako za muda na kiwango cha sigara unazovuta kwa nyakati hizo, kisha panga utaratibu mpya. Kwa mfano kama unavuta sana wakati ukiwa kwenye mawazo hakikisha kuwa unapoanza kufikiria juu ya jambo fulani uwe na kitu mbadala kitachukua nafasi ya sigara. Mfano kahawa au chai? Hakikisha kila penye hamu ya uvutaji unaweka kitu kingine mbadala cha kufanya zaidi ya kuvuta sigara.

*Ondoa masalio ya sigara katika sehemu ambazo unaishi, fua nguo zote na vitambaa ili kuondoa harufu ya sigara katika eneo unalokuwepo. Usikae karibu na mtu anayevuta, usikubali kuwa mshirika wa mvutaji na usiwe mtu wa kuendekeza sana msukumo wa mwili unaotaka uvute, bali kila unapowaza juu ya kuvuta fikiria madhara na nia yako ya kuacha.

*Wafahamishe rafiki zako kuwa umeamua kuachana na uvutaji, ili upate watu wa kuwaonea aibu pale utakapoanguka na kurudia uvutaji wa sigara. Panga tarehe ya kuacha na iwe kwenye kumbukumbu.

*Wakati ukiiendea tarehe hiyo ya kuacha hakikisha unapunguza kiwango cha uvutaji kadiri unavyoisogea siku hiyo. Jipangie muda mrefu zaidi ya kuvuta kulingana na kiwango chako cha uvutaji na kuendelea kuuongeza kila siku ili uzoee kukaa saa nyingi bila kuvuta.

*Fuata ratiba mbadala uliyojiwekea kuziba pengo la uvutaji, kama umepanga kutumia kahawa kila unapokuwa mpweke sebuleni hakikisha unajizoeza ili ikifika tarehe yako ya kuacha usiwe mtu wa kujiuliza cha kufanya nyakati ambazo utakuwa na hamu ya sigara.

*Lengo lako liwe ni kufanikiwa na usikate tamaa utakaposhindwa kufanikisha lengo lako kwa wakati uliojipangia. Mara kwa mara nenda kamuone daktari mshauri ili akupe muongozo zaidi wa kukusaidia na ikiwezekana akupe nafasi ya kuwatembelea wagonjwa waliopata ugonjwa wa kifua kwa sababu ya kuvuta sigara.

Kwa kifupi hizo ni dondoo chache tu za kukusaidia kuachana na uvutaji wa sigara, lakini mara nyingi kinachoweka nguvu za kufanikisha uachaji wa sigara ni utashi wa mtu ambao hutokana na tathimin ya kina ya muhusika na mtazamo wake juu ya sababu za kuacha. Mara nyingi wanaoshindwa ni wale ambao hawakuzitia nguvu sababu za kuacha kwao.
 
KUMBUKA(note)
Siku zote mwanadamu anaongozwa na utashi na kila mwenye kutaka hufanikiwa. Hii ina maana kuwa kama mwanadamu atasema hawezi kuacha kitu fulani, haina maana kama hawezi kwa sababu ameshindwa kujizuia bali ameamua kutokutaka na kinachomshinda ni matokeo ya ya maamuzi yake. Kila anayetaka jambo hufanikiwa na hata wavutao sigara wanaweza kuacha kama wakitaka kufanya hivyo.

namna ya kujiepusha namna ya kujiepusha

. Wanawake wengi kwa kawaida huwa wanahisi uchovu wakati wa ujauzito. Uchovu, kulegea mwili na kuishiwa na nguvu ni jambo la kawaida katika kipindi hicho. Hii ni kwa sababu mwili katika kipindi hiki unatumia nguvu za kiada ili kuunda kiumbe kipya. 
 
Pia wakati huu mwili hutengeneza damu kwa wingi zaidi ili kufikisha chembechembe za chakula kwa mtoto, suala ambalo huufanya mwili ufanye kazi ya ziada na hata viungo vingine muhimu kama vile moyo na vinginevyo. Uzito wa mtoto nao unaoongezeka katika mwili wa mama mjamzito siku baada ya siku, ni sababu nyingine inayomfanya mama mjamzito ajihisi kuchoka. Kuchoka au kiushiwa na nguvu ni tatizo la kawaida hasa katika miezi mitatu ya mwanzo ya mimba. Katika miezi hiyo ya mwanzo ya mimba tatizo hilo husababishwa na mabadiliko ya homoni za mimba mwilini hasa progestrogen na wakati mwingine hali hiyo huongezwa na kichefuchefu na kutapika. 
 
Hali hiyo ya mchoko inatarajiwa kuisha inapoingia miezi mitatu ya pili ya mimba. Lakini pia kuna wengine ambao hali hiyo ya kuchoka huendelea nayo hadi wakati wa kujifungua. Kushindwa kulala vizuri kutokana na kwenda mara kwa mara msalani, au kukosa uzingizi kutokana na ongezeko la ukubwa wa tumbo mwishoni mwa ujauzito, ni miongoni mwa masuala ambayo humfanya mama mjazito ajisikie mchovu na akose nguvu siku nzima.
 
Vilevile mabadiliko ya kifizikia na kisaikolojia ya wakati wa ujauzito humfanya mama mjamzito awe na morali ya chini na kuhisi uchovu wa kimwili na hata kiakili. Sababu nyinginezo zinaweza kutokana na kazi mbalimbali anazofanya mama huyo au pia ukosefu wa lishe inayofaa na ya kutosha kwa ajili ya mwili wake, ambao unahitajia nguvu ya ziada hasa kwa ajili ya uumbaji wa ukamilifu wa mtoto aliye tumboni.
 
La muhimu analoshauriwa mama mjamzito ni kutoogopa na kutotishwa na hali hiyo, kwani inatokana na baadhi ya mabadiliko yanayotokea katika mwili wake. La muhimu ni mama mjamzito kufuata ushauri unaotakiwa ili kukabilina na hali hiyo.
Zifuatazo ni njia za kukabiliana na uchovu wakati wa ujauzito.
 
• Kwanza kabisa mama mjamzito anatakiwa ale vyema. Mama mjamzito anatakiwa ale chakula bora na kamili, chenye kalori 300 au 500 za ziada ikilinganishwa na mtu asiye mjamzito kwa siku. Lakini awe mwangalifu na ni bora akigawe chakula chake katika sehemu ndogo ndogo 5 au 6 (suala hili tumelizunguzia kwa undani katika makala iliyopita ya kiungulia wakati wa ujauzito, tafadhali pitia makala hizo). Anaweza akawa akibeba matunda na mboga mboga kama asusa (snacks) kwa ajili ya kula kila anapohisi njaa popote pale awapo. Lakini ni bora ajiepushe na vyakula vyenye sukari nyingi na caffeine, kwani vyakula hivyo huyeyuka haraka mwilini na kumfanya ahisi njaa mapema.
 
• Mama mjamzito ahakikishe kuwa hana upungufu wa damu. Na kama anao basi atumie dawa za kuongeza damu zinazotolewa na madaktari, au ale vyakula vinavyoongeza damu. Hii ni kwa sababu ukosefu wa madini ya chuma mwilini unaosababisha ukosefu wa damu, ni miongoni mwa sababu zinazomfanya mama mjamzito ahisi kuchoka. Mtu mwenye ukosefu wa damu (Anemia) huhisi kubanwa na pumzi, ongezeko la mapigo ya moyo, udhaifu, kupauka na kizunguzungu. Onana na daktari iwapo una dalili kama hizo.



• Mama wajawazito wanashauri kujipumzisha nyakati za mchana. Ni bora mama mjamzito apumzike kwa kadri anavyoweza wakati wa mchana, baada ya chakula cha mchana au hata kabla ya nyakati za magharibi. Ikiwa unafanya kazi, basi pumzika mara kwa mara japo kwa muda mfupi ili kufanya mwili upate nguvu.
 
• Mama wajawazito wanashauriwa kujitahidi kulala mapema, hasa kama ikiwa inakubidi uamke mara kadhaa usiku kutokana na sababu mbalimbali, kama vile kwenda msalani, kula au kutokana na maumivu.
 
• Kufanya mzoeni husaidia kupunguza uchovu na kuna faida kemkem wakati wa ujauzito. Kahusiana na suala hilo soma makala zilizotangulia.
 
• Mama mjamzito anatakiwa anywe maji ya kutosha. Ukosefu wa maji mwilini huchangia kumfanya mama mjamzito ahisi uchovu.
 
• Usifanye kazi nyingi kutwa nzima, na kama inawezekana ni bora usaidiwe kazi hizo hasa za nyumbani na watu wengine katika familia kama vile watoto, mume ndugu, jamaa na marafiki.
 
• Usikilize mwili wako. Pale unaposikia njaa basi kula na pale unapojisikia uchovu jitahidi upumzike.
 
• Pata ushauri wa daktari iwapo unahisi uchovu wa kupindukia au unachoka kila mara, ili uwe na uhakika kuwa hakuna tatizo au hatari inayoweza kuhatarisha maisha yako na ya mtoto.

ZITTO ZUBERI KABWE (MB) AONGEA BAADA YA KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA

1. Utangulizi 

Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22 Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vyama.
 
Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu


Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama. 


i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu jambo .
  • Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
  • Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam, Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea urais.
  • Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
  • Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.

ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu, na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua. 


iii) Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho. 
 
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi. Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko. 


v) Tuhuma kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae. Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo: 


  • Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania kuzibadilisha
  • Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.


vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao 
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011 kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:


  • Sipokei posho yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka 2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
  • Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000 wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
  • Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.




3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe 
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu nililalamikia mambo matatu yafuatayo:


  1. Kwamba baadhi ya waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu. Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
  2. Kwa kuwa chama kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.




4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za Tanzania. Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo ningetangaza 'maamuzi magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani nchini mwetu. Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo hili.

Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza. Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama chetu.

Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.

Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama daima.

MALINZI AWATEUA MANJI, YUSSUF BAKHRESA KAMATI ZA TFF.

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametangaza wajumbe wa kamati ndogongo (standing committees) wakati zile za haki (judicial organs) na uchaguzi zitaundwa baadaye.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika leo (Novemba 23 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Rais Malinzi alisema kamati hizo zimeundwa kwa mujibu wa katiba ili kuisaidia Kamati ya Utendaji.
Pia ametangaza wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji aliowateua. Wajumbe hao ni Richard Sinamtwa na Ramadhan Nassib, wakati wengine wanaoingia moja kwa moja kwenye Kamati ya Utendaji kutokana na kamati wanazoziongoza ni Dk. Paul Marealle na Saloum Umande Chama.
 
Kamati ya Fedha na Mipango inaongozwa na Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia wakati wajumbe ni Francis Ndulane (Makamu Mwenyekiti), Omari Walii, Eliud Mvella, Said 
 
Muhammed, Geofrey Nyange, Kidao Wilfred, Ayoub Nyenzi, Lina Kessy na Cyprian Kuhyava.
Geofrey Nyange anaongoza Kamati ya Mashindano wakati wajumbe ni Clement Sanga (Makamu Mwenyekiti), Msafiri Mgoyi, James Mhagama, Mohamed Nassoro, Moses Katabaro, Seif Ahmed, Gerald ambi, Davis Mosha, Said George na Nassoro Idrissa.
 
Kinara wa Kamati ya Ufundi ni Kidao Wilfred wakati wajumbe ni Athumani Kambi (Makamu Mwenyekiti), Vedstus Lufano, Blassy Kiondo, Rahim Kangezi, Patrick Kahemele, Daud Yassin, Nicholas Mihayo na Dk. Cyprian Maro.
 
Kamati ya Mpira wa Miguu wa Vijana inaongozwa na Ayoub Nyenzi, Khalid Abdallah (Makamu Mwenyekiti), Ali Mayay, Mulamu Ng’hambi, Apollo Kayungi, Said Tully, Luteni Kanali Charles 
 
Mbuge, Lameck Nyambaya na Ibrahim Masoud.
Lina Kessy anaongoza Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake wakati wajumbe ni Shyrose Bhanji (Makamu Mwenyekiti), Zena Chande, Amima Karuma, Dk. Cecilia Makafu, Zafarani Damoder, Beatrice Mgaya, Sofia Tigalyoma, Martin Mung’ong’o na Engrid Kimaro.
 
Kamati ya Waamuzi inaongozwa na Saloum Umande Chama, Nassoro Said (Makamu Mwenyekiti), Charles Ndagala (Katibu), Riziki Majala, Kanali Isaro Chacha, Paschal Chiganga, Victor Mwandike, Soud Abdi na Zahra Mohamed.
 
Hamad Yahya Juma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi anaongoza Kamati ya Habari na Masoko wakati wajumbe ni Naibu Waziri January Makamba (Makamu Mwenyekiti), Tido Mhando, Yusuf Manji, Yusuf Bakhresa, Samwel Nyalla, Jack Gotham, Fredrick Mwakalebela na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).
 
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inaongozwa na Richard Sinaitwa, Moses Karuwa (Makamu Mwenyekiti), Zacharia Hanspoppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega.
 
Kiongozi wa Kamati ya Ukaguzi wa Fedha ni Ramadhan Nassib wakati wajumbe ni Zitto Kabwe (Makamu Mwenyekiti), Nicholas Magarinza, Jackson Songora, Epaphra Swai, Kalilo Samson, Goodluck Moshi, Golden Sanga na Elias Mwanjala.
 
Dk. Paul Marealle anaongoza Kamati ya Tiba wakati wajumbe ni Dk. Fred Limbanga (Makamu Mwenyekiti), Dk. Mwanandi Mwankemwa, Dk. Nassoro Matuzya, Dk. Eliezer Ndelema na Asha Sadick.

Ijumaa, 22 Novemba 2013

23 KUIWAKILISHA BARA KOMBE LA CHALENJI, MECHI DHIDI YA STARS, ZIMBABWE YAINGIZA MIL 50.

DSC_0918Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 23 watakaoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 27 mwaka huu.
Kilimanjaro Stars iliyotwaa kombe hilo mara ya mwisho mwaka 2010 chini ya Kocha Jan Poulsen, na ambayo imepangwa kundi B katika michuano ya mwaka huu itacheza mechi yake ya kwanza Novemba 28 mwaka dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Machakos.
Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Tanzania Bara ni makipa Deogratius Munishi (Yanga), Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Himid Mao (Azam), Ismail Gambo (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Michael Pius (Ruvu Shooting) na Said Moradi (Azam).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Ramadhan Singano (Simba) na Salum Abubakar (Azam).
Safu ya ushambuliaji inaundwa na Elias Maguli (Ruvu Shooting), Faridi Musa (Azam), Joseph Kimwaga (Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC), Mrisho Ngasa (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC).
Kilimanjaro Stars inatarajia kuondoka Jumatatu (Novemba 25 mwaka huu) kwenda Nairobi kushiriki michuano hiyo itakayoanza Novemba 27 mwaka huu na kumalizika Desemba 13 mwaka huu.   
MECHI DHIDI YA STARS, ZIMBABWE YAINGIZA MIL 50/-
Mechi ya kirafiki ya kimataifa ya FIFA Date kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (The Warriors) iliyochezwa juzi (Novemba 19 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 50,980,000 kutokana na watazamaji 7,952.
Tiketi za kushuhudia mechi hiyo ziliuzwa kwa sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Mgawanyo wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni sh. 7,776,610.17 wakati wa gharama za uchapaji tiketi ni sh. 3,682,560.
Asilimia 15 ya uwanja sh. 5,928,124, asilimia 20 ya gharama za mechi sh. 7,904,166 na asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 1,976,041.
Asilimia 60 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) sh. 17,784,373 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 889,219 ambayo ni asilimia 5 kutoka kwenye mgawo wa TFF.
 
 
Blogger Templates